top of page

Zaidi ya Adhabu ya Viboko: Kufikiria Upya Nidhamu Mashuleni Tanzania!

Writer: Adveline Minja
Adveline Minja
Nov 6
5 min read

By Wisdom Thrives Media | Civic Education. Strategic Commentary. Principled Analysis


Kujenga nidhamu kupitia mazungumzo, mwongozo na uwajibikaji kwa kuheshimu utu wa mwanafunzi ni mjadala chanya wa kumwelimisha mwanafunzi, mzazi, na jamii.
Kujenga nidhamu kupitia mazungumzo, mwongozo na uwajibikaji kwa kuheshimu utu wa mwanafunzi ni mjadala chanya wa kumwelimisha mwanafunzi, mzazi, na jamii.

Je, shule inaweza kuwa na nidhamu imara bila kutumia viboko? Na kama viboko vitaondolewa, walimu, wazazi na wanafunzi wako tayari kwa mabadiliko hayo?

Haya ni maswali muhimu yanayohitaji majibu ya kielimu, na sio ya hisia pekee.


Mnamo Novemba 3, 2026, Mahakama Kuu ya Tanzania ilibatilisha vifungu vya 2, 3 na 6 vya Kanuni za Adhabu ya Viboko Shuleni za mwaka 2002, baada ya kubaini kuwa vinakiuka masharti ya Katiba yanayolinda utu wa binadamu na kukataza adhabu za kikatili, zisizo za kibinadamu au zinazodhalilisha mwanafunzi. Uamuzi huu umefungua ukurasa mpya katika mjadala kuhusu nidhamu mashuleni. Lakini pia umeibua swali kubwa zaidi: Je, tunaondoa viboko pekee, au tunajenga mfumo bora zaidi wa kufundisha nidhamu, uwajibikaji na tabia njema?


Mjadala wa Mabadiliko Ulianza Kabla ya Uamuzi wa Mahakama


Ni muhimu kutambua kuwa suala la kurekebisha sheria na taratibu za adhabu mashuleni lilikuwa tayari limeanza kujadiliwa na Serikali kabla ya uamuzi huu.


Mei 1, 2026, Mussa Mnyeti, akiwakilisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika mkutano wa wadau, alieleza kuwa Serikali ilikuwa ikizingatia mapendekezo ya kupitia upya sheria zinazosimamia nidhamu mashuleni. Alibainisha kuwa suala hilo lingeingizwa katika mchakato wa mapitio ya sera na sheria kwa mwaka wa fedha 2026/27.


Aidha, Septemba 4, 2026, katika mazungumzo na Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Mtoto, ujumbe wa Tanzania ulieleza kuwa adhabu ya viboko ilikuwa imepigwa marufuku Zanzibar, na kwamba Tume ya Kurekebisha Sheria ilikuwa imependekeza kuondolewa kwa adhabu hiyo Tanzania Bara.


Ujumbe huo ulieleza pia kuwa Serikali ilikuwa na mpango wa kuwasilisha muswada bungeni, ingawa kulikuwa na mitazamo tofauti katika jamii iliyohitaji kushughulikiwa. Kauli hizi zinaonyesha kuwa mabadiliko ya mfumo wa nidhamu yalikuwa tayari katika mjadala wa kitaifa kabla ya uamuzi wa mahakama. Hata hivyo, mipango iliyotangazwa kabla ya hukumu si sawa na maelekezo mapya ya utekelezaji baada ya hukumu. Hadi Novemba 6, 2026, hatujathibitisha kuwepo kwa waraka mpya wa Wizara unaoelekeza shule namna ya kutekeleza uamuzi huo.


Hapa ndipo umuhimu wa hatua zinazofuata unapojitokeza: Sheria zinaweza kubadilishwa, lakini walimu, wazazi na wanafunzi wanahitaji kuelewa namna mabadiliko hayo yatakavyotekelezwa katika maisha ya kila siku ya shule.


Nidhamu Sio Sawa na Adhabu

Kwa miaka mingi, baadhi ya jamii zimehusisha nidhamu na adhabu ya mwili. Kwa mtazamo huo, mwanafunzi anayeadhibiwa kwa viboko anaweza kuonekana kuwa amefundishwa nidhamu. Lakini kuna tofauti kati ya mwanafunzi anayetii kwa sababu ya hofu na anayeelewa kwa nini anatakiwa kuwajibika kwa matendo yake.


Nidhamu yenye tija inapaswa kumsaidia mwanafunzi kutambua kosa, kuelewa athari zake, kurekebisha mwenendo na kujenga uwezo wa kufanya maamuzi bora baadaye. Hii

haimaanishi kwamba wanafunzi waachwe wafanye wanavyotaka. Shule zinahitaji sheria, mipaka, uongozi na hatua zinazotekelezwa kwa haki na uthabiti. Swali ni jinsi ya kusimamia hayo bila kuumiza au kudhalilisha mwanafunzi.


Je, Mbinu Zipi Zinafaa na Kwa Umri Gani?


Kwa watoto wadogo, hasa katika elimu ya awali, maelekezo mafupi, ratiba zinazoeleweka, kuonyesha mfano mzuri na kuelekeza upya tabia vinaweza kuwa na manufaa. Katika umri huu, watoto bado wanajifunza kudhibiti hisia, kufuata maelekezo na kuishi na wengine.


Kwa wanafunzi wa shule za msingi, nidhamu inaweza kujengwa kupitia kanuni zilizo wazi, mazungumzo, pongezi kwa tabia nzuri, matokeo yanayohusiana na kosa na nafasi ya kurekebisha makosa.


Kwa wanafunzi wa sekondari, ambao wanakua katika uwezo wa kufikiri na kuwajibika, shule zinaweza kutumia hatua nyingine zinazolingana na uzito wa kosa. Hatua hizo zinaweza kujumuisha onyo la mdomo kutoka kwa mwalimu au uongozi wa shule, kuwekwa katika kipindi maalumu cha uangalizi (detention), kutenganishwa kwa muda mfupi na kundi linalochochea utovu wa nidhamu, au kupewa jukumu maalumu la kurekebisha madhara yaliyosababishwa. Hatua hizi ni za kurekebisha tabia sio adhabu. Marekebisho chanya yanaleta nidhamu.


Kwa makosa yanayojirudia, wazazi au walezi wanaweza kuitwa shuleni ili kushirikiana kuandaa mpango wa kurekebisha na kuboresha mwenendo wa mwanafunzi.


Kwa makosa makubwa yanayohatarisha usalama, kusababisha vurugu wakati wa mafunzo darasani, kukiuka sheria za shule na nidhamu na mwongozo wa darasani kunaweza kumsimamisha masomo mwanafunzi kwa muda kulingana na kuzingatiwa sheria na taratibu za shule. Hatua hii inapaswa kuwa ya uwiano, ya haki, na ya kuambatana na mpango wa kumrejesha mwanafunzi katika mazingira ya kujifunza tabia inayokubalika katika mazingira ya shule.


Hata hivyo, mbinu hizi si lazima ziwe na matokeo mazuri kila wakati. Kuwekwa detention bila mwongozo kunaweza kuwa ni kupoteza muda tu na kumnyima mwanafunzi wakati wake wa kuwa darasani kujifunza. Kutengwa na wenzake kwa namna ya kumdhalilisha kunaweza kuleta madhara pia. Kazi maalumu zisigeuzwe kuwa mateso au kazi hatarishi, bali ziwe na maelekezo ya kubadilisha tabia isiyokubalika kuwa tabia chanya na nidhamu binafsi na hata kwa walimu na shule kwa ujumla. Kumnyima mapumziko muhimu(recess), chakula, maji au mahitaji ya msingi si njia inayofaa ya kujenga nidhamu-ila kumnyima mwanafunzi kile anachokitegemea au kukizoea kama recess/kucheza na wenzake, n.k., wakati amefanya makosa au kokusa nidhamu inafaa ifanyike na maelezo ya kumwelimisha ni kwa nini atakosa hiyo fursa ya recess au kuwa sehemu nyinge mbali na wengine wakati anafanya makosa au kukosa nidhamu. Kwa nama hiyo, mwanafunzi anaelewa ni kwa nini amenyimwa hiki au kile anapokosa nidhamu kama njia ya kumrekebisha.


Hatua ya kinidhamu inapaswa kufundisha uwajibikaji, si kutengeneza aina nyingine ya ukatili. Mbinu hizi zinahitaji pia kuzingatia umri, uwezo wa mwanafunzi, mazingira ya kosa na taratibu halali za shule.


Walimu Wanahitaji Msaada, Sio Maagizo Pekee Tuu

Uamuzi wa mahakama hauwezi wenyewe kutatua changamoto za usimamizi wa tabia darasani. Mwalimu anayesimamia darasa kubwa, lenye wanafunzi wenye mahitaji na tabia tofauti, anahitaji mafunzo, muda, msaada wa uongozi na taratibu zinazotekelezeka. Ni muhimu pia kutofautisha makosa ya kawaida ya kitabia, matatizo yanayojirudia, changamoto za kihisia au kujifunza, na vitendo vikubwa vinavyohatarisha usalama. Hali hizo haziwezi kutatuliwa kwa adhabu moja. Shule zinahitaji mifumo ya kusikiliza wanafunzi, kushirikisha wazazi, kutatua migogoro, kutoa ushauri na kufuatilia mabadiliko ya tabia.


Je, Wazazi na Wanafunzi Wana Wajibu Gani?

Wazazi wanaweza kusaidia kwa kuelewa kanuni za shule, kuzungumza na watoto wao kuhusu wajibu wao na kushirikiana na walimu pale matatizo yanapotokea. Wanafunzi nao wanahitaji kuelewa kwamba haki zao zinaambatana na wajibu wa kuheshimu sheria za shule, taratibu/kanuni za darasani, kuwaheshimu wengine, kutunza mali na heshima ya shule, kutowahatarisha usalama wa wenzao, walimu, au wa shule.


Kukomesha adhabu ya viboko hakumaanishi kufuta uwajibikaji wa mwanafunzi.

Vilevile, kudai nidhamu hakupaswi kuwa sababu ya kupuuza utu na usalama wa mtoto.


Mtazamo wa Nurture Forward Foundation


Kwa mtazamo wa Nurture Forward Foundation (NFF), mjadala huu unapaswa kuwa sehemu ya mazungumzo mapana kuhusu elimu, malezi, maendeleo ya mtoto na uwezo wa taasisi zetu kujenga tabia njema zenye maadili ya kuelewana na kuheshimiana.


Mabadiliko ya nidhamu yanahitaji zaidi ya kubadilisha kanuni. Yanahitaji kuandaa walimu, kuwaelimisha wazazi, kuwashirikisha wanafunzi na kuweka mifumo ya uwajibikaji inayolinda mazingira ya kujifunzia na kulea kitabia chanya.


Shule yenye nidhamu si lazima iwe shule ambayo wanafunzi wanaiogopa. Inaweza kuwa shule ambayo wanafunzi wanaelewa wajibu wao, wanaheshimu wengine na wanawajibishwa kwa haki na wanatambua nidhamu na tabis zinazokubalika sio tuu shuleni, bali na kwa jamii pia.


Uamuzi wa mahakama umefungua mjadala. Hatua inayofuata ni kuhakikisha kuwa mbinu mbadala za nidhamu zinaeleweka, zinafundishwa na zinatekelezwa kwa ufanisi.


Swali kwa jamii


Je, tunawaondolea walimu viboko tu, au tunawajengea pia uwezo wa kusimamia nidhamu kwa mbinu zinazofaa zaidi?


Walimu, wazazi, wanafunzi na wadau wa elimu—ni mbinu zipi mnazoona zinaweza kujenga nidhamu bila kuathiri utu na usalama wa mwanafunzi, mazingira na sifa za shule?



 
 
 

Comments

Rated 0 out of 5 stars.
No ratings yet

Add a rating
Wisdom Thrive Media log for independent media and civic education

We are a knowledge-driven company dedicated to sharing practical ideas that inspire growth, learning, and meaningful living. Through insightful content and thoughtfully crafted products like our signature collection of books.

© 2025 by CultivateCreativeCo.

Powered and secured by Wix

Contacts

Germantown, Maryland - US
Dar es Salaam, Tanzania 

​

+1 240 805 4193

​

care@wisdomthrives.com

  • Instagram
  • Facebook
  • LinkedIn
  • X
  • Whatsapp

Newsletter

bottom of page