Zaidi ya Mafanikio ya Masomo—Maandalizi ya Maisha Baada ya Kumaliza Shule!

Na Nurture Forward Foundation (NFF) | Kukuza Uwezo. Kuimarisha Familia. Kujenga Mustakabali.

Kuhitimu elimu ya sekondari ni hatua muhimu katika safari ya elimu ya kijana. Hatua hii inakmilisha miaka mingi ya kujifunza, juhudi binafsi, uwekezaji wa familia, pamoja na kujitolea kwa walimu na taasisi za elimu. Hata hivyo, pamoja na sherehe za kuhitimu, matokeo ya mitihani, na vyeti vya masomo, bado kuna swali muhimu la kiuuliza:
Je, vijana wameandaliwa kwa kiwango gani kukabiliana na maisha baada ya kumaliza shule?
Kwa vijana wengi, kipindi hiki cha kughitimu sasoma ya secondari au vyuo ni kipindi cha mpito kinachoambatana na hali ya kutokuwa na uhakika wa maisha. Baadhi ya vijana hulazimika kuamua endapo wataendelea na elimu ya juu, mafunzo ya ufundi na ustadi wa kazi mbalimbali, na wengine hawana marikira kabisa juu yah atua itakayofuata baada ya kuhitimu masomo ya shuleni. Wengine hukabiliwa na changamoto za kifedha, uhaba wa fursa za ajira, mabadiliko ya mahitaji ya soko la ajira, au ugumu wa kutambua vipaji, uwezo, na mambo wanayopenda.
Mafanikio ya masomo huweka msingi muhimu, lakini hayamaanishi moja kwa moja kwamba vijana wamejengewa ujuzi wa vitendo, kujiamini, ujasiria mali, rasilimali, au mwongozo kamili unaohitajika kufanya maamuzi sahihi kuhusu mustakabali wao.
Changamoto wanazopitia vijana katika Mpito wa Kumaliza Shule na Kuelekea Maisha Halisi.
Changamoto zinazowakabili vijana wakati wanapomaliza shule zinajidhihirisha pia katika takwimu za kimataifa kuhusu ajira.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2025, takribani asilimia 20.4 ya vijana wenye umri wa miaka 15–24 duniani kote hawakuwa katika ajira, elimu, wala mafunzo mwaka 2024. Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana kilikuwa karibu mara tatu ya kiwango cha watu wazima.
Ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), Global Employment Trends for Youth 2024, nayo liliangazia hali ya kutokuwa na uhakika wa ajira kwa vijana katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako takribani robo tatu ya vijana wanaofanya kazi hawakuwa na ajira zenye uhakika na ulinzi wa kutosha.
Matokeo haya yanaonyesha kuwa kuwawezesha vijana kupata elimu ni jambo la msingi jambo la msingi, ingawa elimu peke yake haitoshi kuwapatia au kudhamini ajira. Vijana wanahitaji pia njia zinazounganisha elimu na ujuzi wa vitendo, fursa zenye maana, ushiriki katika shughuli za kiuchumi na maendeleo binafsi.
Ni muhimu pia kutambua kwamba ukosefu wa ajira na uhaba wa fursa haviwezi kuhusishwa tu na upungufu wa ujuzi wa mtu binafsi. Hali ya uchumi, upatikanaji wa mtaji, mifumo ya soko la ajira, tofauti za kijiografia na upatikanaji wa ajira zenye staha pia huathiri matarajio na fursa za vijana.
Kuunganisha Elimu, Uwezo, na Ujuzi wa Kutenda kwa Vitendo
Uwezeshaji wa vijana huanza pale maarifa yanapogeuzwa kuwa uwezo wa vitendo, fursa za kujipatia kipato, na ujuzi wa kifedha unaowawezesha kusimamia rasilimali kwa uwajibikaji na ubunifu.
Elimu ya fedha huwasaidia vijana kuelewa na kusimamia fedha, kujenga tabia nzuri za kupanga bajeti na kuweka akiba, kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, na kutambua uhusiano kati ya kupata kipato, matumizi, kuweka akiba na kuwekeza kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
Utafiti wa kitaalamu umeonyesha mafanikio ya kazi na kipato yanaletwa na fikra za kina, mawasiliano yenye ufanisi, uwezo wa kutatua matatizo, ujuzi wa kidijitali, uwezo wa kukabiliana na mabadiliko, kufanya kazi kwa ushirikiano , kuwa na uamuzi wa busara, kuchagua kwa makini, kijiamini na kujaribu ujasiriamali.
Tafiti hizi za kitaalamu huwa na maana zaidi pale vijana wanapopata fursa za kuzitumia kwa vitendo.
Kwa mfano, mwanafunzi anayevutiwa na sekta ya ukarimu na huduma za wageni anaweza kunufaika na uzoefu wa vitendo katika maandalizi ya utengenezaji wa vyakula, huduma kwa wateja, utalii au uendeshaji wa biashara ndogo ndogo za kutoa huduma kwa watu.Mwingine anayevutiwa na teknolojia ya kidijitali anaweza kujifunza utengenezaji wa video, uundaji wa maudhui ya kidijitali, mawasiliano ya mtandaoni au matumizi yenye uwajibikaji ya teknolojia zinazoibuka.
Uzoefu wa aina hii unaweza kuwasaidia vijana kuelewa matarajio ya mazingira ya kazi, viwango vya kitaaluma na kitaalamuzinazohitajika katika maeneo ya kazi mbali mbali, ushirikiano, pamoja na uhusiano kati ya ujuzi na fursa za kiuchumi.
Hata hivyo, kuwa na akili au ujuzi hakumaanishi moja kwa moja kupata ajira au kipato. Vijana wanahitaji pia taarifa kuhusu mahitaji ya soko, mafunzo bora ya kujiboresha, mitandao ya kitaaluma na fursa halisi za kutumia uwezo wao.
Kugeuza Maarifa ya Darasani kuwa Vitendo: Mfano wa Kutia Moyo kutoka Shule ya Sekondari Uroki

Wakati wa ziara katika Shule ya Sekondari Uroki, wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Tanzania, tarehe 10 Novemba 2026, wawakilishi wa Nurture Forward Foundation (NFF) taasisi ya binasfi inayojuhusisha na maswala ya kuboresha elimu na afya kwa watoto, kwa familia, na jamii kwa jumla, walivutiwa na maelezo ya mwanafunzi mmoja wa Kidato cha Kwanza kuhusu jinsi alivyogeuza maarifa aliyojifunza darasani kuwa shughuli za vitendo za kujipatia kipato.
Mwanafunzi huyo alieleza kuwa baada ya kujifunza somo la biashara darasani, aliamua kutumia maarifa aliyoyapata darasani kwa kuanzisha bustani ndogo ya mboga. Alilima mboga na kuuza mboga hizo, hivyo kujipatia fedha za ziada zilizoongeza kiasi cha fedha za matumizi binafsi alizokuwa akipewa na wazazi wake.
Juhudi zake hazikuishia hapo!
Baada ya kujifunza somo jingine kuhusu utayarishaji wa vitafunio rahisi, alianza kutengeneza vitafunio kama maandazi, skonzi na keki, ambazo aliziuza kwa watu majirani na anakoishi.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, kipato alichopata kutokana na shughuli hizo kimemwezesha kukidhi mahitaji yake binafsi ya matumizi bila kuendelea kutegemea fedha za matumizi kutoka kwa wazazi wake.
Kilichowavutia wawakilishi wa NFF si tu kwamba mwanafunzi huyu mdogo alikuwa amegundua njia za kujipatia fedha, bali uwezo wake wa kutambua fursa, kutumia maarifa ya darasani na kujenga uwezo wa vitendo huku akiendelea na masomo yake.
Uzoefu wake unaonyesha jinsi kujifunza kunavyoweza kuvuka mipaka ya mitihani na masomo ya darasani. Kupitia shughuli hizi, amepata uzoefu wa awali katika uzalishaji, ujasiriamali, mahusiano na wateja, uwajibikaji wa kifedha na utatuzi wa matatizo.
Mfano huu pia unaonyesha umuhimu wa mazingira ya elimu yanayowahamasisha wanafunzi kuchunguza namna maarifa wanayopata yanavyoweza kutumika katika maisha ya kila siku.
Kwa vijana wengine, uzoefu wake unahamasishaa na unatoa ujumbe muhimu: kwamba, si lazima kusubiri hadi kuhitimu masomo ndipo mtu aanze kutambua na kutumia fursa zenye maana. Kwa mwongozo unaofaa, rasilimali zilizopo, na dhamira ya kujituma, wanafunzi wanaweza kuanza kujenga uwezo na uzoefu wenye manufaa wakiwa bado shuleni.
Mafanikio makubwa zaidi si tu kwamba alipata fedha, bali alijifunza kugeuza maarifa kuwa vitendo.
NFF inatambua juhudi za mwanafunzi huyu kama mfano wa kutia moyo unaoonyesha uhusiano kati ya elimu, ujuzi wa vitendo na maandalizi ya maisha baada ya shule.
Simulizi yake inatukumbusha kwamba kuwaandaa vijana kwa ajili ya maisha ya kesho kunamaanisha pia kuwasaidia kutambua na kukuza uwezo walio nao leo.
Nafasi ya Ulezi wa Kitaaluma, Ushauri na Mwongozo wa Kazi
Ushauri na mwongozo kwa wanafunzi unaweza kuwasaidia vijana kuchunguza uwezo wao, mambo wanayopenda, matarajio yao na njia mbalimbali zinazopatikana kabla ya kufanya maamuzi makubwa kuhusu elimu au kazi.
Mwongozo wenye ufanisi unapaswa kuwahamasisha vijana kujiuliza maswali ya maana:
Ninapenda nini na nina uwezo gani? Ni njia zipi za elimu au mafunzo ya ufundi zinazopatikana? Ni ujuzi gani wa vitendo unaoweza kuongeza fursa zangu? Nitahitaji rasilimali gani za kifedha? Ni njia gani mbadala ninazoweza kuzingatia iwapo chaguo langu la kwanza halitapatikana?
Kutoa ushauri na mwongozo si kuwafanyia vijana maamuzi kuhusu maisha yao ya baadaye. Bali ni kuimarisha uwezo wao wa kutathmini njia mbalimbali, kutafuta taarifa za kuaminika, kuelewa changamoto zinazoweza kujitokeza na kufanya maamuzi ya busara na ufahamu.
Mwongozo wa taaluma na kazi unapaswa pia kutambua kwamba mafanikio yanaweza kupatikana kupitia njia tofauti. Elimu ya chuo kikuu, mafunzo ya ufundi na stadi za kazi, ajira, ujasiriamali, sekta za ubunifu na shughuli za maendeleo ya jamii zote zinaweza kuwa njia zenye maana, kutegemea mazingira ya mtu binafsi na fursa zinazopatikana.
Familia, Shule na Jamii Zinazoshirikiana Kwa Pamoja
Kuwaandaa vijana kwa maisha baada ya shule kunahitaji ushirikiano kati ya familia, walimu, washauri, waajiri, taasisi za mafunzo na huduma za jamii.
Wazazi na walezi wanaweza kuwahamasisha watoto na vijana kujenga uwajibikaji, uelewa wa fedha, uwezo wa kufanya maamuzi na mazungumzo ya kweli kuhusu matarajio yao ya kielimu na kikazi.
Shule zinaweza kuimarisha uhusiano kati ya masomo ya kitaaluma na matumizi yake kwa vitendo, huku waajiri na mashirika ya kijamii wakichangia kupitia fursa zinazofaa za kujifunza katika mazingira ya kazi, ushauri na mwongozo, maonyesho ya ujuzi na upatikanaji wa taarifa kuhusu fursa zinazoibuka.
Vijana wenyewe wanapaswa kuwa washiriki wachangamfu katika mchakato huu. Mambo wanayopenda, uzoefu wao, ndoto na mitazamo yao vinapaswa kuzingatiwa katika aina ya msaada wanaopatiwa, na wao kuwa mstari wa mbele kuwa na fikra chamya na endelevu.
Maandalizi yenye maana hutokea pale vijana wanaposaidiwa, si tu kutambua fursa zilizopo, bali pia kuzielewa, kuzitathmini na kuzifuatilia.
Dhamira ya NFF katika Kusaidia Vijana Kupitia Hatua za Mpito wa Kielimu
Katika Nurture Forward Foundation, Programu ya Ushauri, Ulezi wa Kitaaluma na Huduma za Ushauri Elekezi katika Elimu (Educational Mentoring, Coaching & Consulting Program — EMCCP), pamoja na vipaumbele vyetu vya Uwezeshaji wa Vijana na Maandalizi kwa Maisha ya Kesho, vinaakisi umuhimu wa kuunganisha kujifunza, maendeleo binafsi, ujuzi wa vitendo na maamuzi sahihi kuhusu elimu.
Mtazamo wetu unatambua kwamba vijana wanahitaji zaidi ya kutiwa moyo kufaulu kitaaluma. Wanahitaji pia mahusiano yenye msaada, fursa za kuchunguza na kukuza uwezo wao, pamoja na mwongozo unaozingatia hali halisi ya dunia inayobadilika.
Kuimarisha uhusiano huu ni sehemu muhimu ya kuwaandaa vijana kupitia hatua mbalimbali za mpito wa kielimu, kushiriki kwa tija katika jamii na kuchangia maendeleo katika maeneo wanamoishi.
Kuwaandaa Vijana kwa Maisha, Sio Kwa Mitihani Tuu

Vyeti na sifa za kitaaluma vinaendelea kuwa mafanikio yenye thamani. Vinawakilisha maarifa, nidhamu na juhudi, na vinaweza kufungua milango muhimu ya elimu na taaluma. Hata hivyo, madhumuni mapana ya elimu yanapaswa pia kujumuisha kuwaandaa vijana kufanya maamuzi yenye uwajibikaji, kukabiliana na mabadiliko, kujenga uwezo wa vitendo na kutafuta fursa zenye maana.
Kwa hiyo, swali si kwamba mafanikio ya kitaaluma yana umuhimu? Swali ni kwamba mifumo ya elimu na ya huduma inafanya vya kutosha kuunganisha mafanikio hayo ya maisha baada ya shule?.
Mafanikio ya elimu hayapaswi kuishia kwenye kile vijana wanachokijua wanapoondoka shuleni. Yanapaswa pia kuonekana katika kiwango ambacho wanasaidiwa kutumia maarifa hayo, kutambua na kutumia fursa, na kujenga mustakabali wao.
Kama wazazi, walimu, washauri na wanajamii, tuna wajibu wa pamoja wa kusaidia kufanya kipindi hiki cha mpito kuwa chenye uelewa, ushirikishwaji na mwelekeo wenye maana.
Ni maarifa gani ya vitendo au stadi gani ya maisha unayoamini kila kijana anapaswa kuwa nayo kabla ya kuhitimu elimu ya sekondari?
Nurture Forward Foundation | Nurturing Lives. Empowering Families. Uplifting Communities.
Like. Comment. Share. Follow Nurture Forward Foundation: https://www.nurtureforwardfoundation.org
Marejeo
Umoja wa Mataifa (2025). Ripoti ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2025 — Lengo la 8: Kazi Zenye Staha na Ukuaji wa Uchumi.
Shirika la Kazi Duniani (ILO, 2024). Global Employment Trends for Youth 2024: Decent Work, Brighter Futures.
UNICEF. Education and Skills Development.




Comments